Tuesday, 18 November 2014

WATU 600 WAWEKWA KARANTINI KWA HOFU YA MAMBUKIZI MALI


Nchini Mali, watu 600 wako chini ya uchunguzi wa maambukizi ya Ebola wakati huu nchi hiyo ya Afrika Magharibi ikiweka mikakati kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa huo hatari.
 
Wakati hayo yajikiri, viongozi wa serikali walikutana Jumatatu Novemba 17 kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa hasa katika mpaka wake na Guinea, nchi iliyoathiriwa zaidi na ugonjwa wa Ebola.

Hadi sasa watu wawili wamepoteza maisha nchini Mali baada ya kuambukizwa Ebola.
Rais Ibrahim Boubacar Keita, amezuru katika mpaka wa nchi hiyo na Guinea katika eneo la Kouremale na kutoa wito kwa wenyeji kuhakikisha kuwa wanasaidia kupambana na ugonjwa huu kwa kutoa ripoti kwa yeyote anayeshukiwa kuambukizwa.

Umoja wa Ulaya umeahidi kutoa Dola Milioni 15 kwa nchi ya Mali, Senegal na Cote d'Ivoire ili kuweka mikakti ya kuzuia kusambaa kwa Ebola kutoka nchi jirani kama Guinea, Liberia na Siera Leone.

Shirika la afya duniani, limesema zaidi ya watu elfu tano wamepoteza maisha katika nchi za Afrika Magharibi kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Wednesday, 5 November 2014

UKEKETAJI WA WASICHANA WADORORESHA ELIMU LAMU


Ukeketaji wa wasichana unaoendelea kutekelezwa kila uchao katika jamii ya Boni kaunti ya Lamu umetajwa kama changamoto kuu inayosababisha kudorora kwa viwango vya elimu katika eneo hilo.
 
Haya ni kwa mujibu wa afisa mkuu wa elimu ya afya,jinsia na jamii katika kaunti hiyo Hamisi Kaviha ambapo amesema hali hiyo inaendelea kuzidi na kusababisha wasichana wengi kupachikwa mimba miongoni mwao 15 kutoka shule ya msingi ya Bargoni.

Akizungumza na wanahabari wakati wa ziara yake katika eneo la Boni Kaviha ameeleza kuwa afisi yake ilibaini kwamba shughuli hiyo hutekelezwa kwa watoto walio kati ya umri wa miaka 9 na 10 hasa kwenye sherehe za mwezi December.

Amedokeza kuwa baada ya wasichana hao kukeketwa wao hujihisi kwamba wako katika nafasi ya kupata kuolewa mapema kabla ya umri wao kufika.

Hata hivyo amesema wameweka mikakati ya kushirikiana na machifu pamoja na viongozi wengine ili kuwakamata wale ambao wanahusika na maafa hayo.